WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amevitaka viwanda vya sukari nchini kuongeza mikakati ya uzalishaji zaidi ili mwaka 2020 Tanzania iwe imefikia kiwango cha kuzalisha asilimia 100 ya mahitaji yake.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo jana (Jumanne, Agosti 02, 2016) wakati
alipotembelea kiwanda cha sukari cha Mtibwa kilichoko mkoani Morogoro
ambapo amesisitiza viwanda vya ndani vizalishe zaidi ili kupunguza
uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.
Amesema
Serikali imejikita katika kuimarisha na kulinda viwanda vya ndani
nchini hivyo ni vema viwanda vya sukari vikaweka mikakati ya kuzalisha
kwa wingi ili kuondokana na uagizaji wa bidhaa hiyo kutoka nje.
“Kiwango
cha mahitaji ya sukari nchini ni zaidi ya tani 400,000, nimeiagiza Bodi
ya Sukari kukaa na wataalamu wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na
kufanya utafiti ili tujue mahitaji halisi ya sukari,” alisema.
Waziri
Mkuu amesema Serikali imeweka mkakati wa kulinda viwanda vya ndani kwa
kuziongezea kodi bidhaa zinazotoka nje ambazo zinazalishwa na viwanda
vya ndani ikiwemo sukari hivyo wenye viwanda hawana budi kuzalisha kwa
wingi zaidi.
Hata
hivyo Waziri Mkuu amewataka wamiliki wa viwanda vya sukari nchini kutoa
motisha kwa wakulima wa nje kwa kununua miwa yao kwa bei nzuri na
kuwalipa kwa wakati ili nao wanufaike na uwepo wa viwanda hivyo na kuwa
walinzi wa uwekezaji huo.
Kwa
upande wake Meneja Uhusiano Mwandamizi wa kiwanda hicho, Ibrahim Juma
amesema kwa sasa kiwanda kinazalisha tani 20,000 kwa mwaka na
wanatarajia kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 70,000 ifikapo mwaka
2021.
Juma
alisema uzalishaji wa sukari kiwandani hapo ulipungua kutokana na
uingizwaji wa sukari kutoka nje hivyo aliipongeza serikali kwa kudhibiti
uingizwaji holela wa sukari kutoka nje jambo litakalosaidia ukuzaji wa
viwanda vya ndani.
Meneja
huyo alisema kuwa kwa sasa wameanza upanuzi wa mashamba kiwandani hapo
ambapo wanatarajia kuongeza hekta 400,000 lengo likiwa ni kutimiza ndoto
ya Serikali ya kuifanya Tanzania ijitosheleze katika uzalishaji wa
sukari.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, AGOSTI 02, 2016.
TANGAZO LA NDANI===
Facebook Blogger Plugin by SAMCHARDTZ




Chapisha Maoni